Watoto 196 pewa mimba ktk kipindi cha miezi 12 Wilayani Iramba!
Eric Buyanza
April 1, 2024
Share :
Watoto wa kike 196 wamepewa ujauzito na wengine 69 kuolewa wilayani Iramba, mkoani Singida katika kipindi cha miezi 12 ya mwaka jana.
Ofisa Ustawi wa Jamii wilayani Iramba, Happiness Alex, amebainisha ukatili huo katika kikao cha Kamati ya Ulinzi wa Mwanamke na Mtoto.
Alex amesema kati ya watoto hao waliopewa ujauzito, 18 ni wanafunzi na watoto walio nje na taasisi ni 179.
Amesema kuwa matukio ya ulawiti kwa watoto wa kiume yanazidi kuongezika; kwa mwaka 2022 yalikuwa matano na 2023 yaliyoripotiwa 19, hali ambayo inaipa kamati kazi ya ziada kunusuru jamii.
Alex amesema sababu za kuongezeka kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ni umaskini, mila na desturi kandamizi, matumizi mabaya ya utandawazi, mmomonyoko wa maadili na malezi hasi ya wazazi na walezi.
Mkuu wa Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi, Nduara Mbalamwezi amesema matukio yaliyoripotiwa polisi ni 82 kwa mwaka 2023.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho, ameagiza wajumbe wa kamati hiyo kuwa makini na wageni wanaokuja wilayani mwao na ajenda mbalimbali ambazo hazina maadili kwa sababu ndio wanachochea vitendo hivyo.
"Mkiona mambo hayo yanafanyika, toeni taarifa kwenye mamlaka husika ili hatua zichukuliwe haraka kwa ajili ya kukomesha vitendo hivi ambavyo kimsingi vinawaathiri watoto ambao ni nguvukazi ya taifa baadaye," amesema.
Katiba ya Tanzania (1977), Sheria ya Ulinzi wa Mtoto (2009) na mikataba ya kimataifa ambayo nchi imeiridhia vinazuia ukatili wa kingono dhidi ya watoto.
NIPASHE