Watumia shilingi milioni 11, kufanya mazishi ya 'gari la familia'
Eric Buyanza
November 28, 2024
Share :
Katika hali ya kushangaza familia moja huko nchini India imefanya mazishi ya kifahari kwa ajili ya gari lao pendwa aina ya Suzuki Wagon R, mazishi ambayo yalihudhuriwa na takriban watu 1,500.
Familia ya Polara inayotoka Kijiji cha Padarshinga huko Gujarat, ilidumu na gari hilo kwa miaka 18 huku wakiamini lilikuwa ni gari la bahati kwao na hivyo walitaka kuliaga kwa heshima zote badala ya kuliacha tu likichakaa nje ya nyumba kama inavyofanyika kwa magari mengine.
Akina Polara walichimba kaburi la futi 15 kwenye eneo lao na kisha gari hiyo iliteremshwa polepole likiwa limefunikwa kwa maua na kupambwa kwa vitambaa vya rangi mbalimbali huku muziki wa kihindi ukipigwa.
Kisha familia hiyo ilifanya matambiko kadhaa kama sehemu ya sherehe ambayo inasemekana iligharimu zaidi ya dola 4,500 (sawa na milioni 11 za kitanzania).
“Gari hili lilikuwa zaidi ya gari..ilikuwa sehemu ya safari yetu kuelekea mafanikio. Badala ya kuiuza, tulitaka kuiheshimu kwa kumbukumbu ya kudumu kwa vizazi vijavyo,” alisema mmiliki wa gari hilo aliyefahamika kwa jina la Sanjay.
Baada ya matambiko ya kimila kumalizika, kaburi hilo lilifunikwa kwa udongo.
Sanjay ambaye ana kampuni ya ujenzi anasema ana mpango wa kupanda mti juu ya kaburi hilo ili kukumbusha vizazi vijavyo kwamba pale ni mahali palipo pumzika 'gari la bahati' ya familia.