Waumini wasali nje kisa mgogoro wa ardhi
Sisti Herman
April 21, 2024
Share :
Zaidi ya waumini 200 wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) lililopo Ngulelo Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha wamefanya ibada nje ya nyumba ya mtu baada ya kukuta kanisa lao limefungwa na kuzungushiwa mabati kutokana na mgogoro wa ardhi.
Eneo la kanisa hilo lilizungushiwa mabati wiki iliyopita na mtu anayetajwa kuwa mmiliki wa eneo hilo, baada ya kushinda kesi kuhusu madai ya kuvamiwa eneo la familia yake na kuendelezwa bila kibali cha familia.
Katika shauri hilo, Askofu wa Kanisa hilo la KKAM, Philemon Mollel maarufu kama Monaban ndiye aliyedaiwa kuvamia eneo hilo na kujenga kanisa lililokuwa linatumiwa na waumini hao.
Wakizungumza leo na waandishi wa habari Jumapili Aprili 21, 2024, waumini hao wamesema uhuru wa kuabudu umeporwa na watu wanaodai eneo hilo ni lao, na wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati mgogoro huo.
Kwa upande wake, mmoja wa wanafamilia wanaodai eneo lao kuvamiwa, William Mollel amesema wameamua kuzuia shughuli zozote kuendelea katika eneo lao lililovamiwa.
“Baba yetu alituchia hili eneo sisi familia yake, na Monaban alikuja kumrubuni aliyekuwa msimamizi wetu wa mirathi akadai amenunua. Hii ni Mali ya familia huwezi kununua kwa mtu mmoja, hivyo amfuate aliyempa hela arudishiwe hela zake lakini kwa sasa tumeshakua na tumekuja kumiliki mali zetu wenyewe,” amesema William.
Chanzo; Mwananchi