Waziri Mkuu aamua kupumzika kugombea ubunge.
Joyce Shedrack
July 2, 2025
Share :
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ametangaza rasmi kupumzika kugombea tena Ubunge wa Jimbo la Ruangwa, mkoani Lindi, baada ya kuliongoza jimbo hilo kwa takribani miaka 15 mfululizo tangu alipopewa ridhaa na wananchi wa Ruangwa mwaka 2010.

Hatua hiyo imekuja siku chache tu baada ya Majaliwa kutangaza Bungeni, Juni 26, 2025, kuwa anapanga kugombea tena ubunge wa jimbo hilo, akisisitiza kuwa anaendelea kuhitaji ridhaa ya wananchi. Hata hivyo, kauli hiyo sasa imebadilika rasmi.
"Ninatambua wakati mwingi nimekuwa nje ya jimbo nikilitumikia taifa lakini wana Ruangwa wameendelea kuniunga mkono. Nitumie nafasi hii kusema asanteni sana na ninamuomba Mwenyezimungu azidi kuimarisha mshikamano uliopo kati yetu sote. Ninaomba kuwajulisha kuwa ninakuja kuchukua fomu ya kuomba ridhaa yenu tena.", alinukuliwa bungeni.
Uamuzi wa Majaliwa umepokelewa kwa hisia tofauti, huku baadhi ya wachambuzi wa siasa wakiutaja kuwa ni uamuzi wa busara na wa kiungwana, hasa baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka 10 cha Uwaziri Mkuu tangu alipoteuliwa mwaka 2015.
Hatua hii pia inakuja wakati chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikiwa katika harakati za ndani za uteuzi wa wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Zoezi hilo limeanza Juni 28 na linatarajiwa kukamilika leo Julai 2, 2025.