Waziri Mkuu mpya wa Senegal atangaza Baraza la Mawaziri
Eric Buyanza
April 6, 2024
Share :
Waziri Mkuu wa Senegal Ousmane Sonko ametangaza serikali mpya itakayokuwa na mawaziri 24 na manaibu 5. Hiyo ni siku chache baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo kufuatia kuchaguliwa kwa mshirika wake mkuu Bassirou Diomaye Faye kuwa rais wa taifa hilo la Afrika Magharibi.
Sonko amesema rais Faye --aliyeapishwa siku ya Jumanne kuiongoza Senegal baada ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa rais wa Machi 24-- amewaidhinisha mawaziri wote waliopendekezwa.
Utendaji wa Baraza hilo jipya la mawaziri utafuatiliwa kwa karibu hasa kutokana na ahadi kubwa za mageuzi zilizotolewa na rais Faye wakati wa kampeni. Miongoni mwa hizo ni kuzifanyia ukaguzi mkubwa sekta za nishati ya mafuta, gesi pamoja na uchimbaji madini. Miongoni mwa walioteuliwa kuwa mawaziri ni Cheikh Diba atakayeongoza wizara ya fedha huku Abdourahmane Sarr ametangazwa kuwa waziri wa uchumi.
Majenerali wawili wameteuliwa kuongoza wizara ya mambo ya ndani na ile ya Ulinzi.
DW