Waziri wa Somalia azuiliwa kuingia Kenya, aishia Airport
Eric Buyanza
July 27, 2026
Share :

Waziri wa masuala ya nchi katika Ofisi ya Rais, Abshir Bukhaari, ameripotiwa kuzuiwa kuingia nchini Kenya na baadaye kurejeshwa Mogadishu, kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali.
Maafisa wa uhamiaji wa Kenya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi wanadaiwa kumzuia kuingia nchini siku ya Jumapili kutokana na pasipoti ya Kenya aliyokuwa akisafiria.
Serikali za Somalia na Kenya hazikuwa zimetoa kauli rasmi kuhusu tukio hilo.
Taarifa hiyo inafuatia tukio jingine lililotokea takribani mwezi mmoja uliopita (Juni 24), lililomhusisha Naibu Waziri Mkuu wa Somalia, Jibril Abdirashid Haji, ambaye pia aliripotiwa kunyimwa kuingia nchini Kenya na kurejeshwa Somalia kutokana na madai kuwa alikuwa na pasipoti ya Kenya iliyopatikana kwa njia ya udanganyifu.
Naibu Waziri Mkuu huyo aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa JKIA kwa ndege ya Shirika la Saacid Airlines kutoka Mogadishu na kuwasilisha pasipoti halali ya kidiplomasia ya Somalia pamoja na visa ya kuingia Kenya.
Taarifa zinasema maafisa wa uhamiaji walimtilia shaka baada ya kushukiwa kuwa pia alikuwa na pasipoti ya Kenya iliyopatikana kwa njia isiyo halali.
Vyanzo vinavyofahamu suala hilo viliviambia vyombo vya habari vya ndani kuwa afisa huyo wa Somalia alikiri kuwa na pasipoti ya Kenya, lakini alikataa kuikabidhi, akisema suala hilo linapaswa kushughulikiwa kupitia mchakato wa mahakama.
Mvutano huo ulisababisha Haji kupelekwa katika eneo la mapumziko la wageni maalumu la uwanja wa ndege wakati uchunguzi ukiendelea, kabla ya baadaye kusindikizwa kupanda ndege ya Shirika la Daallo Airlines iliyokuwa ikielekea Mogadishu, na hivyo kunyimwa rasmi ruhusa ya kuingia nchini Kenya.
Hadi wakati huo, serikali za Kenya na Somalia hazikuwa zimetoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo.
BBC





