YAMAL AWAGOMEA FIFA: Amkataa Rodri, amtaja Messi kuwa bora zaidi
Eric Buyanza
September 19, 2026
Share :

Kinda wa klabu ya FC Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania, Lamine Yamal, ameingia kwenye vichwa vya habari baada ya kupingana waziwazi na maamuzi ya FIFA kuhusu mchezaji aliyestahili tuzo ya Mchezaji Bora (Golden Ball) kwenye mashindano ya Kombe la Dunia ya 2026.
Katika mahojiano yake mapya kabisa na kituo cha Movistar, Yamal amesisitiza kuwa nahodha wa Ajentina, Lionel Messi, ndiye aliyekuwa mchezaji bora zaidi wa mashindano hayo, licha ya FIFA kumtunza kiungo mwenzake wa Uhispania, Rodri. Hatua hii inakuja wiki chache baada ya Uhispania kuifunga Ajentina goli 1-0 katika fainali kali iliyopigwa nchini Marekani.
Licha ya kubeba ubingwa huo akiwa na kikosi cha Uhispania, kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 hakusita kueleza mahaba na heshima yake kwa Messi.
"Kwangu mimi, Leo Messi alikuwa mchezaji bora wa Kombe la Dunia kwa sababu ya kila kitu anachowakilisha na kila kitu alichokifanya uwanjani," alisema Yamal kupitia mahojiano hayo.
"Hakuna aliyetarajia mchezaji wa umri wa Leo (miaka 39) kuonyesha vitu vikubwa vya kiwango kile. Hivyo kwangu mimi, yeye ndiye aliyekuwa bora zaidi."
Uamuzi wa FIFA wa kumpa Rodri tuzo hiyo ulitokana na uwezo wake mkubwa wa kutawala kiungo na kuiongoza Uhispania kupata ushindi kwenye mechi zote bila kupoteza. Hata hivyo, takwimu binafsi za Lionel Messi katika umri wa miaka 39 zilikuwa za kustaajabisha, kwani alimaliza mashindano akiwa amepachika mabao 8 na kutoa pasi za mabao (assists) 4.
Yamal hakumkosoa Rodri moja kwa moja, lakini maoni yake yanatajwa kuamsha mjadala mzito duniani kote kuhusu nani hasa alistahili kubeba tuzo hiyo ya heshima.





