Yanga kujenga ghorofa la Bilion 5.5 Kariakoo.
Joyce Shedrack
September 9, 2026
Share :
Klabu ya Yanga imetangaza kuingia ubia wa ushirikiano na benki ya Azania (Azania Bank) wa kujenga jengo la ghorofa 12 lenye thamani ya Shilingi bilioni 5.5 katika Mtaa wa Mafia na Nyamwezi, jijini Dar es Salaam.

Rais wa klabu ya Yanga, Eng. Hersi amesema Mradi huo wenye lengo la kuimarisha miundombinu na kuongeza thamani ya mali za klabu hiyo unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha takribani miezi 12, na klabu hiyo itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba utekelezaji unafanyika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyowekezwa.
“Ninayo furaha kutangaza rasmi kwamba Azania Bank ndiyo benki itakayotoa ufadhili wa ujenzi wa mradi huu. Makubaliano haya yataipa taasisi yetu fursa ya kupata fedha zinazohitajika kwa ajili ya kujenga na kukamilisha mradi huu.
Tunatambua kwamba fedha hizi ni mkopo na kwa hiyo tunapaswa kuhakikisha kwamba mradi huu unazalisha mapato yatakayowezesha kulipa deni hilo kwa wakati.
Tunaamini kabisa kwamba kwa sababu ya eneo ambalo jengo hili limejengwa pamoja na matumizi yake, kutakuwa na vyanzo mbalimbali vya mapato vitakavyowezesha mradi huu kujiendesha na kulipa mkopo.
Tunawashukuru sana Azania Bank kwa kuamini katika mradi huu” Eng. Hersi Said, Rais wa klabu ya Yanga SC.





