Yanga yafa kiume ikiyaaga mashindano ya klabu bingwa afrika
Eric Buyanza
April 6, 2024
Share :
Klabu ya Yanga jana ilikufa kibabe baada ya kuilazimisha klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kutafuta ushindi kupitia mikwaju ya penalti.
Sundowns walijikatia tiketi ya kucheza nusu fainali kwa kupachika wavuni penalti 3-2 za Yanga katika mchezo wa duru ya pili wa robo fainali uliopigwa mjini Pretoria.
Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bila kufungana kama iliyokuwa kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa mjini Dar es Salaam mwishoni mwa juma lililopita.
Mamelodi Sundowns ambao hawakuonesha mchezo wowote wa kushangaza, sasa watasubiri kufahamu iwapo watacheza nusu fainali dhidi ya ama ASEC Mimosa ya Ivory Coast au miamba Eseperance ya Tunisia zitakazokutana leo mjini Abidjan.
Kwa ujumla Sundowns walitawala mchezo wote wa Ijumaa usiku lakini hawakuwa na umakini wa kuamua ni wakati gani hasa walipaswa kushambulia.
Hali hiyo haikumnyima usingizi mlinda mlango wa Yanga Djigui Diarra.
Baada ya kipindi cha kwanza kilichoshuhudia shambulizi moja tu la uhakika kutoka kwa Sundowns, vijana wa Yanga walianza kuonesha makeke na hasa kasi ya mshambuliaji raia wa Burkina Faso Stephane Aziz Ki iligeuka kitisho cha wazi.
Dakika 59 Ki aliamini ameipatia Yanga nafasi ya kusonga nusu fainali pale mkwaju wake mkali ulipompiga golikipa Williams na kugonga kingo ya ndani ya goli.
Hata hivyo teknolojia ya VAR iliamua kwamba halikuwa goli.