Zelensky amtimua kazi mkuu wa majeshi, Oleksandr Syrskyi
Eric Buyanza
July 22, 2026
Share :

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amemwondoa Mkuu wa Majeshi ya Ukraine, Oleksandr Syrskyi, kutoka kwenye wadhifa wake.
Hatua hiyo imekuja siku chache tu baada ya kuondolewa kwa Waziri wa Ulinzi aliyekuwa maarufu, Mykhailo Fedorov, hatua iliyosababisha maandamano katika maeneo mbalimbali nchini humo.
Awali kulikuwa na uvumi kwamba kuondolewa kwa Fedorov kulihusiana na mgogoro kati yake na Syrskyi, na baadaye taarifa hizo zikathibitishwa.
Fedorov, mwenye umri wa miaka 35, amekuwa akisifiwa kwa kuleta mageuzi makubwa katika Wizara ya Ulinzi, kuimarisha uwezo wa jeshi la Ukraine na kuongoza juhudi za kupambana na rushwa.
Kwa upande mwingine, Syrskyi, mwenye umri wa miaka 60, anaonekana na wengi nchini Ukraine kama kamanda mwenye mtazamo wa kijeshi wa enzi za Umoja wa Kisovieti, ambaye hakuwa tayari kutekeleza mabadiliko makubwa ndani ya jeshi.
Nafasi yake imechukuliwa na Jenerali Mykhailo Drapatyi, mwenye umri wa miaka 43, ambaye anajulikana kwa uzoefu wake mkubwa vitani na umaarufu miongoni mwa wanajeshi.
"Nitafanya kazi kwa uwajibikaji, kwa umakini wa hali ya juu, na kwa heshima kwa wale wote wanaolinda nchi yetu leo," Drapatyi aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Pia alimshukuru Syrskyi "kwa kazi yake ya muda mrefu ya kuimarisha jeshi la Ukraine," akiongeza kuwa, "Nilikulia ndani ya jeshi hilo."
Katika ujumbe wa video aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii usiku wa Jumanne, Rais Zelensky alimshukuru Syrskyi kwa mchango wake katika kampeni za kijeshi, ikiwemo nafasi yake muhimu katika kutetea kwa mafanikio mji mkuu wa Kyiv wakati wa siku za mwanzo za uvamizi kamili wa Urusi mwaka 2022.
BBC





