Zelensky, Netanyahu wakutana na Trump huku vita vikiendelea
Eric Buyanza
July 29, 2026
Share :

Rais Donald Trump amefanya mikutano tofauti na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, mikutano ambayo Ikulu ya Marekani ilielezea kuwa ya "kujenga na yenye tija".
Viongozi hao wawili walikuwa Washington kuhudhuria maziko ya Seneta Lindsey Graham, ambaye alikuwa mfuasi mkubwa wa Israel na mtetezi wa misaada ya Marekani kwa Ukraine, ambaye alifariki dunia mapema mwezi huu.
Zelensky na Trump walijadili matumaini ya Kyiv kwamba Marekani ingesaidia kuimarisha mifumo yake ya ulinzi wa anga, ingawa hakuna ahadi rasmi iliyotolewa hadi sasa.
Kwa upande wake, Netanyahu aliwasili wakati ambapo uhusiano kati ya Marekani na Israel ulikuwa umetetereka kutokana na mitazamo tofauti kuhusu Iran.
Kabla ya ziara hiyo, ilitarajiwa kuwa Zelensky angemshinikiza Trump kutimiza ahadi aliyotoa katika mkutano wa kilele wa NATO mwezi huu ya kuipa Ukraine kibali cha kutengeneza makombora ya Patriot ya kuzuia mashambulizi ya anga.
Kwa muda mrefu Ukraine imekuwa ikitaka makombora ya Patriot ya Marekani; Kyiv inasema makombora hayo yanaweza kutumika kuilinda miji ya Ukraine dhidi ya mashambulizi yanayoongezeka ya ndege zisizo na rubani na makombora ya masafa marefu kutoka Urusi kote nchini humo.
Hata hivyo, mkutano huo uliofanyika kwa faragha ulimalizika bila tangazo lolote thabiti kuhusu msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine.
Trump aliandika kwenye mtandao wa Truth Social kwamba mkutano huo "ulienda vizuri sana!"
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Zelensky alimshukuru rais wa Marekani kwa "kila tunachofanya kwa pamoja kulinda maisha ya raia wa Ukraine".
Aliongeza kuwa wawili hao walijadili kuhusu vibali vya Patriot na "mawazo kadhaa ambayo yanaweza kusaidia".
"Tulizungumzia pia masuala ya kidiplomasia," aliandika. "Ni muhimu mchakato wa kidiplomasia ufufue nguvu mpya."
Katika ujumbe mwingine tofauti, Zelensky amesema alikutana na wawakilishi wa kampuni ya Marekani inayotengeneza zana za kijeshi ya Lockheed Martin ili kujadili "kuendeleza zaidi ushirikiano wao.
BBC





