Zimbabwe yaachia sarafu mpya kupambana na mfumuko wa bei
Eric Buyanza
April 5, 2024
Share :
Zimbabwe, iliyotumbukia katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi kwa takriban miaka ishirini, imeidhinisha sarafu mpya ili kujaribu kupambana na mfumuko wa bei, Benki Kuu ya nchi hiyo imetangaza siku ya jana Ijumaa.
"Kuanzia leo, benki zitabadilisha pesa zinazotumika kwa sasa (Dola za Zimbabwe) kuwa sarafu mpya iitwayo Zimbabwe Gold, ZiG," Mkuu wa benki kuu ya Zimbabwe, John Mushayavanhu, amesema katika mkutano na waandishi wa habari.
Mwaka 2008, mfumuko wa bei ulifikia kiwango ambacho benki kuu ilitoa noti ya trilioni ya dola za Zimbabwe. Kisha serikali ililazimika kuachana na fedha za ndani, huku dola ya Marekani ikiwa fedha rasmi. Dola ya Zimbabwe ilifufuliwa mwaka wa 2019. Lakini Wazimbabwe wengi wanapendelea kuendelea kutumia dola ya Marekani, hasa kwa mishahara na katika ulimwengu wa biashara.